MASOMO YA MISA, JANUARI 29, 2017 MASOMO YA MISA, JANUARI 29, 2017 DOMINIKA YA 4 YA MWAKA A MWANZO: Zab. 106:47 Ee Bwana Mungu wetu, utuokoe, utukusanye kwa kututoa katika mataifa, tulishukuru jina lako takatifu, tuzifanyie shangwe sifa zako. SOMO 1 Sef. 2:3, 3:12 – 13 Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na masikini, nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya. Neno la Mungu… Tumshukuru Mungu. WIMBO WA KATIKATI Zab. 146:6b – 10 (K) Mt. 5:3 (K) Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Huishika kweli milele. Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa. (K) Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki; Bwana huwahifadhi wageni. (K) Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K) SOMO 2 1Kor. 1:26 – 31 Ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana. Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu. SHANGILIO Yn. 14:5 Aleluya, aleluya, Tomaso akamwambia Bwana, Sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia? Aleluya. INJILI Mt. 5:1 – 12a Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini war oho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Share on Google Plus

About CLETUSKAMANYI BLOG

0 comments:

Post a Comment